Sisi ni vijana wa Kitanzania tulioamua kujumuika na wana maendeleo katika kulisukuma gurudumu hilo kwenye nyanja hii ya lugha yetu hadhimu ya Kiswahili. Waswahili husema "titi la mama ni tamu, katu halinishi hamu." Hakika hii ni bayana, pale tunapoendelea kujinoa zaidi ili kuwaletea elimu kupitia tovuti hii, tukiwajuza na kuwahabarisha yale mnayoyajua na msiyoyajua yahusuyo lugha yetu ya Kiswahili.

Tulianzisha kulitekeleza hili jukumu kwa sababu tuliona kuwa nasi pia tunaweza kutoa mchango katika kukidumisha na kukikuza Kiswahili. Tukachagua njia hii, kwa kuwa sio rahisi kwa mgeni kuifahamu maana ya baadhi ya maneno yatumikayo mitaani mwetu ambayo ni maneno mapya na yasiyo fasaha au ni ya zamani ila yametoholewa maana mpya.

Kamusi ya Kitaa, ni kazi ya sanaa ya kitaa kinachoongea.

Lugha ni chombo kikuu cha mawasiliano katika jamii yoyote. Lakini katika Kizazi hiki kipya lugha yetu inaendelea kuongezeka misemo na maneno mengine mapya kila siku yakitofautiana maana na matumizi kutoka watu wa sehemu moja na nyingine na kuleta kutokuelewana kwa usahihi na huku tukipoteza kabisa baadhi ya maneno ya Kiswahili fasaha. Hivyo basi, kwa kutambua hilo, tumeona tuwaletee tovuti hii ya Kamusi Ya Kitaa kwa lengo la kutuunganisha pamoja tukifundishana na kukumbushana maana na matumizi sahihi ya lugha yetu ya Kiswahili, na kwa mwanafunzi au mgeni wa lugha ya Kiswahili kujifunza lugha yetu ya mitaani. Karibu ujumuike nasi kwa kutukosoa na/au kutushirikisha maneno yoyote mapya au ya zamani ambayo ungedhani ingefaa na wengine wayajue. Karibu sana!


WAASISI NI:

Kindo Emmanuel;

Mhasisi/Mchoraji/Msanii/Mshairi.

Emmanuel Kindole, Maarufu kama "KINDO" Nilizaliwa mjini Iringa mwaka 1989 na kuhamia jijini Dar es Salaam mwaka 1997. Nilisoma Shule ya Msingi Amani, Shule ya Sekondari Dar es Salaam na Kujiunga na Chuo Cha Ufundi Don Bosco kilichopo Msasani.

Kwasasa nimeajiriwa na ofisi ndogo inayojihusha na Upigaji Picha iliyopo mkoani Kigoma wilaya ya Kasulu.

Kitaalamu ni Msanifu Picha (Graphics Designer) pia ni Mshairi, Mtunzi wa Riwaya na Mchoraji.

Napendelea kusikiliza muziki hapa Hip Hop, Reggae na R&B, pia kusoma vitabu, kutazama filamu na kusafiri.

Fabian C. Mwakabanje;

Mhasisi/Mkurugenzi/Mwalimu/Mshairi/Mwanaharakati

Kazi ngumu sana hata kwa mwandishi kujiandikia kama ilivyo kwa mnenaji mzuri kujiongelea, ila ukweli ni bayana kuwa hakuna kazi au shughuli nyepesi kwenye kuishi maisha ya hapa ulimwenguni. Basi, nisamehe kwa kutofuata sheria au kanuni za uandishi kwasababu kuna mwalimu wangu aliniambia ni vigumu kutembea bila kupinda juu ya mstari ulionyooka, lazima utapinda tu.

Shughuli ninazojivunia kuzitenda katika maisha ni chache na zenye manufaa kwa jamii yangu; ya kwanza ni mwalimu wa kujitolea ambaye ninaanzisha na kuzisimamia klabu za kujisomea vitabu (book clubs) kwenye shule za msingi, awali na za upili chini ya mwamvuli wa taasis isiyo ya kiserikali Zuri Foundation, ya pili nayo ni uendeshaji na usimamizi wa miradi yetu midogo midogo itokanayo na mradi huu wa KAMUSI YA KITAA, nazisaka na kuzikusanya taarifa sahihi, nafundisha Kiingereza kwa wazawa na Kiswahili kwa wageni.

Pia ni mwandishi, mhariri, mshauri juu ya elimu na maswala yahuhusuyo masoko katika biashara ya utalii, na mtunzi wa mashairi katika wovuti www.babananiii.wordpress.com

AHSANTE SANA!

imeundwa Kwa upendo Tanzania na Argentina | 2024